Categories: Caricature

Kagame : Mchawi wa amani au mjuzi wa kuvuruga vita ?

Partagez

Hata kama makubaliano ya amani kati ya DRC na Rwanda yamesainiwa mjini Washington, hali ya usalama mashinani haijabadilika hata kidogo. Picha ya kuchokoza inayosambazwa kwenye mitandao inaleta maswali mapya: je, Kagame anamaanisha kweli amani, au bado anachezea moto wa vita vya mashariki ?

Kwenye picha yenye ujumbe wa maana, Paul Kagame anaonyeshwa kama mchawi mwenye fimbo iliyovunjika, mbele ya waraka ulioandikwa “Makubaliano ya Amani kati ya DRC na Rwanda”. Kando yake, kuna vivuli vya watu wenye bunduki wakionekana kuwakilisha makundi ya waasi wanaoendelea kuharibu hali ya usalama mashariki mwa nchi.

Mbele yake, raia wa Kongo aliyevaa vazi la taifa, amesimama mikono kifuani, anasema kwa kejeli: “Kila mara ni uchawi uleule usioleta suluhisho…” Maneno haya yanatoa ujumbe kwamba kuna pengo kubwa kati ya makubaliano kwenye karatasi na hali halisi inayoendelea kwa wananchi.

Tarehe 27 Juni 2025, DRC na Rwanda walisaini makubaliano ya amani Washington, chini ya usimamizi wa Marekani. Lengo lake ni kumaliza vita ya mashariki: kusitisha mapigano, kuheshimu mipaka, na kuvunja makundi ya waasi. Mpango wa pamoja wa usalama ulipendekezwa pia.

Lakini wiki moja tu baadaye, Kagame alitoa hotuba akiwa Kigali, akisema wapo wanaoshindwa kutekeleza yale walikubaliana. Alisisitiza kuhusu FDLR waasi wa Kihutu walioko Kivu akisema kuwepo kwao ni hatari kwa Rwanda.

Hata hivyo, watu wengi DRC hawaamini kauli hizo. Wanasema ni mbinu ya kuficha ukweli, hasa wakati ambapo Rwanda inatuhumiwa kwa kuunga mkono waasi wa M23 wanaopigana na wanamgambo wa Kongo huko Kivu Kaskazini. Mapigano bado yanaendelea, watu wanatoroka makwao, na hali inazidi kuwa mbaya.

Picha hii inawakilisha ukweli ambao watu wengi wa mashariki wanauelewa kwa moyo: maneno peke yake hayatoshi. Bila vitendo vinavyoendana na makubaliano, amani itabaki kuwa ndoto tu. Wakati viongozi wanazungumza meza ya mazungumzo, ni wananchi wa kawaida wanaolipa bei ya vita visivyokwisha.

Ismaël Masiya Akilimali

Leave a Reply

Votre adresse e-mail ne sera pas publiée. Les champs obligatoires sont indiqués avec *

Dans la même catégorie